Makala

NYOKA MWENYE HATARI KUPITA WOTE

NYOKA MWENYE HATARI KUPITA WOTE

Imewekwa na - October 16, 2020

YA WALIMWENGU 001

NA: George Iron Mosenya

Simu: 0655 727325

_________________
 

Habari za wakati huu mabibi na mabwana..... Mkipata muda nyie mabibi mjiulize kwanini upande wa pili hawajaitwa ‘mababu’ wanaitwa ‘mabwana’. Msikae kimya aisee! Ikibidi muandamane ilimradi tu majibu yapatikane.

Ya maandamano nawaachia nyie, mtaamua katika kikao chenu. Mimi hapa nawaletea kile kipengele chetu pendwa kabisa, kiitwacho YA WALIMWENGU!! Hiki kikiwa ni kipengele ambacho kitakuwa kikikujuza mambo mbalimbali yanayojiri ama yamewahi kujiri ulimwenguni.

Na leo nateta nawe kuhusu nyoka! Achana na yule nyoka mpole sijui alimshawishi Hawa ale tunda halafu ampe na Adam. Hapa nazungumzia nyoka hatarishi kulikoni wote katika bara letu la Afrika.

WAZUNGU huko walimwita Black Mamba, lakini kwa sisi waswahili akatokea muhenga mmoja akamuita KOBOKO, sijafahamu bado kwanini walimuita Koboko. Ila nitafuatilia... kwa sasa hata wewe muite na umwelewe kwa jina la KOBOKO.

HAYA SASA TWENDE PAMOJA.

_________________

KWANINI BLACK! Usije ukakutana na mjusi mweusi ukapiga makelele ukasema umekutana na Black mamba. Hapana, huyu nyoka wala hata sio lazima awe mweusi, kisa tu anaitwa BLACK, wapo wa kijivu na wa njano. Hiyo Black inatokana na kinywa chake pamoja na ulimi hivi vyote ni vyeusi tii! Na ndiye nyoka pekee mwenye hali hii ya weusi wa kinywa na ulimi!

 

HATARI YA SUMU YAKE IPOJE?

Tone moja, Ndiyo! Tone moja tu la sumu yake linatosha kupoteza uhai wa mwanadamu mtu mzima mwenye afya tele, jiulize wasiokuwa na afya inahitajika robo tone au?

Halafu, katika kinywa cheusi cha huyu nyoka, kila muda awe amelala ama anatambaa, kuna jumla ya matone kumi na mawili ambayo yapo tayari kuangamiza mtu. Kwa hiyo watu kumi na mbili wenye afya tele wanaweza kuangamizwa na nyoka mmoja tu kwa mapigo ya kufuatana.

HAUWEZI KUPONA?

Aaaah! Kuna watu wana bahati bwana wee, anaweza akapigwa na KOBOKO na bado akapona, lakini hatabaki kuwa kama alivyokuwa awali. Nyoka huyu sumu yake huathiri sana ubongo wa mwanadamu. Kuna dalili kubwa sana ukipona ukawa tahira a.k.a mwendawazimu AU Kipakatoka.

 

NINAWEZA KUMKIMBIA?

Hebu nisome kwa makini hapa kabla hujaamua kukimbia. Kwanza utajuaje kuwa sasa nipo mbele ya KOBOKO, wakati anataka kushambulia hutoa mlio kama tairi la gari linalotokwa na upepo! Ile shhhhhhhhhhhhhhhhhhhhh!

Sasa ukishasikia hivi, wewe muombe tu Mungu wako, akurehemu. Usikimbie maana huwezi kumkimbia KOBOKO, huyu nyoka ana kasi ya ajabu mno. Narudia usikimbie, ni heri ubaki umeganda na atagundua kuwa wewe sio hatarishi kwake, ila kitendo cha kuunyanyua mguu na kujifanya Usain Bolt, umekwisha!

 

AAAH! MIMI NINA MBIO BWANA NITAKIMBIA!!

Sawa je unaweza kukimbia umbali wa kilometa 19 ndani ya saa zima! Yaani ndani ya dakika 60 tu uwe umekimbia kilometa 19. Kama unaweza kuuvuka mwendo huu basi utaweza kumkimbia KOBOKO, maana huu ndo mwendo ambao anaweza kukimbia. Na ukiachana na hilo la kukimbia kwa mwendo kasi, labda nyoka pekee anayemzidi KOBOKO uwezo wa kufikiria ni yuleyule aliyempa Eva/Hawa lile tunda kule katika bustani ya Eden! Vinginevyo, hakuna Nyoka mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri kumzidi!

 

AKIKATIZA BARABARANI NIMGONGE AU?

Rejea nilichoainisha hapo juu, Nyoka huyu ana uwezo mkubwa sana wa kufikiri. Wewe na Leseni yako Class ‘D’ tena unaendesha gari la shemeji, usijifanye wewe ni mjuaji kuliko KOBOKO ilimradi umfurahishe shemeji yako.

Koboko haji barabarani bahati mbaya, keshaona upenyo wa kukushambulia. Sasa wewe jikaze halafu ufie kwenye gari la shem!

Ukimuona simamisha gari, subiri ajiondokee!

ANA MAAJABU GANI MENGINE?

Nimekueleza kuwa anaweza kukimbia kwa mwendo kasi wa hatari. Hapo unajiambia, “Aaah! Huyu ujanja wake si ni kwenye majani tu, nitakimbilia kwenye barabara ya vumbi huko!”.

Chukua hii! Koboko hakimbii kama nyoka wa kawaida kwa kutambaa mwili mzima, yeye anakimbia huku robotatu ya mwili wake ikiwa juu, yaani ukiangalia upesiupesi ni kama anakimbia huku amesimama.

Huyu hakutishi, bado unaleta jeuri mlimwengu???  Shauri zako!

HAJALI KUHUSU KIZAZI CHAKE:

Eeeh na ukali wake anapandwa kama kawaida tu... hakunaga mjanja huko nd’o maana vichaa wanabeba mimba pia. Kwani wewe hakuna mwalimu wa kike alikuwa mkali huko shuleni kwenu, baadaye unasikia yupo likizo ya uzazi. Unajiuliza iliwezekanaje aisee!

Kwa KOBOKO huko, hutaga mayai kumi na tano hadi ishirini kwa awamu moja. Baada ya kutaga kitu hana ni muda wa kukaa karibu na mayai yake eti asubiri watoto wake.

Koboko ujeuri anaanza tangu anaanza maisha. We jiulize mayai yanaachwa hapo yatajitotoa yenyewe! Vitoto havipate malezi ya baba wala mama, vinaachaje kuwa jeuri!

Na kikishajitotoa tu, kinakuwa tayari na sumu mdomoni inayoweza kuondoa uhai watu wazima watatu.

Ukisikia mtoto wa nyoka ni nyoka nd’o hii hapa sasa! Wewe uje uokote mayai porini huko uyaweke mfukoni yajitotoe black mamba, ung’atwe ufe tukuzike kudadeki zako!

 

KWANI HAYO MAKINDA YANAKUWA NA UKUBWA GANI MI HATA SIYAOGOPI!!

Sawa, unaifahamu rula, eeh! Najua hesabu ulikuwa hauipendi, nahauiwezi hadi sasa. Lakini si ulikuwa unatumia rula kupiga mstari? Ilikuwa na urefu wa sentimeta 30 si ndio? Najua utajikubalisha tu ili niendelee.....

Sasa kinda la KOBOKO linajitotoa likiwa na urefu wa sentimeta 50 hadi 51. Na baadaye hukomaa hadi kufikia urefu wa mita mbili na nusu!

Vipi bado hauogopi?

Ukipiga hatua zako kumi na nne za kutembea, ndo urefu wa Black Mamba aliyekomaa! Wala sio mzito sana, ni kilo moja na nusu tu ya nyama! Ila hilo balaa lake sasa....

 

HUYU KIUMBE ANAISHI KWA MUDA GANI?

Akijitotoa mwaka huu 2020 ataishi hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wakati Magu anaachia Ikulu, kisha ataishi tena mpaka mwaka 2030 wakati bunge linavunjwa na Raisi atakayekuwa amemrithi Magu, halafu tena ataishi ili kutazama huyu raisi atafanya nini katika miaka yake mingine miwili ikulu mnamo mwaka 2032.

Noma eeh! Ee Noma sana, anaishi kwa miaka kumi na miwili!  Ambapo utakuwa umeolewa na kuachika mara tatu... kisha utasema sitaki tena kusikia mambo ya ndoa! Halafu ghafla unajitangaza kuwa wewe ni kungwi.

 

HAWA VIUMBE KWANI TANZANIA WANAPATIKANA.

Ndugu zangu wa Tabora, na Nzega huko, Igunga sijui Ziba, Nkinga hadi kijiji kiitwacho Ulaya. Aisee huko ndo KOBOKO wanapatikana kwa wingi, ila popote pale hawa mabalaa wanaweza kupatikana. Ni wewe tu kuwa makini!

 

Mabibi na mabwana! Nawatakia wakati mwema!! Tuendelee kukutana tena na tena katika vipengele vyetu mbalimbali katika Application yako bora kabisa ya HADITHI.

Naitwa, George Iron Mosenya (Mlimwengu)

Whatsapp: 0655 727325