Makala

MJUE SARAH BAARTMAN

MJUE SARAH BAARTMAN

Imewekwa na - June 16, 2020

SARAH BAARTMAN “SAARTIJIE”:
UZURI WA UMBO LAKE WAWA CHANZO CHA MATESO ULAYA HADI MAUTI.

 

NA: HUSSEIN OMARY MOLITO


Takribani maisha yote ya Sarah yaligubikwa na mateso na udhalilishaji wa hali ya juu. Sarah, alizaliwa Afrika ya Kusini mnamo mwaka 1789, mama yake mzazi alifariki Sarah angali mdogo kabisa, yapata miaka miwili tu, na baba yake ambaye alikuwa mfugaji kama kazi ya kumpatia fulusi, alifariki Sarah alipovunja ungo. Baada ya muda kidogo, Sarah alibarikiwa kupata mtoto wa kiume, ila baba wa kichanga chake hicho, aliuwawa kikatili na mdachi (kaburu) kwa kisa ambacho hadi hivi sasa bado hakijulikani, ila kama ilivyo ada, ni uonevu uleule wa watu weusi dhidi ya watu weusi.
Ingawa Sarah hakujua kusoma wala kuandika, mnamo Octoba 1810 Sarah alitia sahihi mkataba na mganga wa maswala ya upasuaji aliyeitwa William Dunlop (mzungu) ambaye aghalabu shughuli zake alifanya kwenye meli, pia Daktari huyo alikuwa na swahiba ambaye yeye alikuwa chotara, jina lake ni Hendrick Cesars. Watu hawa wawili, Sarah alikutana nao mahala alipokuwa akifanya kibarua kama mfanyakazi wa kazi za ndani. Walivutika sana na Umbo na Sarah, wakamrubuni kuwa wangeenda nae Uingereza kushiriki katika matamasha mbalimbali na angejipatia fedha nyingi zaidi.
Ukubwa wa maumbile ya Sarah, hasa makalio na mapaja yake – ni kutokana na hali tu ya kibaiolojia ambayo inawakuta wanawake wa kiafrika hasahasa kutoka kabisa la Khoisan, hali hii inaitwa “Steatopygia” ambayo husababisha mlundikano wa mafuta katika makalio na mapaja kwa kiasi kikubwa tu. Hii ni kawaida kwa wanawake wengi kutoka nchi za kusini mwa Afrika kama Botswana, Eswatini, Afrika ya Kusini, Leshotho na kadhalika. Baada ya Sarah kurubunika na kutia sahihi mkataba ule, madhalimu wale wawili kumbe walikuwa na mpango wao wa dhambi isiyoweza kusahaulika, waliazimia kutumia maumbile ya Sarah kama chanzo cha mapato, kumtembeza uchi barani ulaya kama kivutio.
Sarah, alipofikishwa tu London, alianikwa uchi katika kumbi kubwa inayoitwa London’s Piccadilly kama kivutio kwa mabwanyenye na watu wa kawaida kulipia kama kumtazama.
Sote tunajua, wanawake wa kizungu toka enzi hadi leo, maumbo yao sio kama ya wanawake wa kiafrika kwenye kipengele cha mvuto. Kwa Ulaya Umbo la Sarah ilikuwa ni kivutio haswa cha aina yake, kwa maana hawakuwahi kuona mtu mwenye umbo kama lile, tena la asili. Majiji makubwa kama Paris na London yalimtambua vyema Sarah, walimchapichika jina la ‘Hottentot Venus’.
Wakati wa maenesho Sarah alivikwa kiguo cha kubana (Skin tight) ili kumchora vyema maungo yake, pia alivikwa manyonya ya tausi kama mapambo, shanga zenye rangi mchanganyiko na pia alikuwa na kiko mdomoni. Matajiri walilipia wa maonesho binafsi hasa majumbani mwao na sehemu nyingine za siri, na wengine walilipia fedha nyingi kumgusa tu alipokuwa jukwaani. Jina walilompa Sarah alipofikishwa ulaya ‘Hottentot’ bado linatumika hadi leo nchi Afrika kusini kuwadhalilisha wanawake kutoka makabila ya ‘Khoikhoi’ na ‘San’ ambao kwa pamoja huitwa ‘Khoisan’.
Serikali ya Uingereza ilitia sahihi mswada wa kupiga marufuku biashara ya utumwa mnamo mwaka 1807, ila haikusitisha utumwa mwenyewe, licha ya kwamba wanaharakati wa maswala ya haki za binadamu walipigia sana kelele swala la Sarah kuhodhiwa pasi na matakwa yake, ila madhalimu wale wawili hawakuwahi kufungwa kwa ukatili wao ingawa kesi ilifunguliwa. Mabwana wale hawakufungwa kwakuwa hata Sarah mwenyewe alisimama upande wao kutoa ushahidi mahakamani, na alisema kuwa yeye mwenyewe aliridhia kufanyiwa vile.
Bado kuna maswali mengi sana miongoni mwa wana historia duniani kuhusu kesi ya Sarah. Bado watu wanahoji kuwa je ilikuwa ni hiari au lazima kwa Sarah kuwa mnenguaji akiwa uputu mbele ya kadamnasi barani Ulaya? Kama alilazimishwa, kwanini hakuwa mwenye kutoa ushahidi ambao ungemsaidia kuepukana na kadhia yote hiyo. Je, ni vipi ikiwa Sarah alitishiwa maisha yake endapo angetoa ukweli mahakamani? Kesi hii hadi leo ni ngumu kwa watu kung’amua ukweli, ila wengi miongoni mwa wanahistoria wa Afrika, wanasema Sarah ameonewa kutokana na misingi ya rangi ya ngozi yake, hata hivyo alikuwa nchi ya kigeni hivyo hakujihisi huru kusema anachotaka kuhofia maisha yake.
Baada ya kesi, Sarah alizoeleka sasa, umaarufu wake ukaanza kudorora, ila bado aliendelea kufanya ziara nchini Uingereza na Ireland. Mnamo 1814 alihamia Paris na moja ya mdhamini wake, Cesars. Kule Paris akawa maarufu maradufu tena, alipenda sana kunywa mvinyo baa moja maarufu iliyoitwa Cafe de Paris na alidhuria ghafla mbalimbali pia. Mdhamini wake Cesars, alirudi Afrika ya Kusini, Sarah Baartman alibaki Paris chini ya Uangalizi wa mtu mmoja ambaye alihusika na maonesho ya wanyama wa mwituni. Sarah alibadili jina akaitwa Reaux.
Huku Paris Sarah alikuwa mlevi na mvutaji nguli wa sigara na madawa ya kulevya, na kwa mujibu wa historia, Sarah alifanya ukahaba na watu mbalimbali ikiwemo na mtu huyo ambaye alihusika na maonesho ya wanyama. Sarah alikubali kuchorwa na wachoraji mbalimbali pia alikubali kufanyiwa utafiti na wanasayansi ila kwa sharti moja, alikataa kubaki mtupu kabisa mbele yao wakati wanafanya hivyo, ingawa walitamani iwe hivyo.
Sarah alifariki akiwa na umri wa miaka 26, inasemekana kuwa chanzo cha kifo chake ni magonjwa kama Pheumonia, Syphiliis (Kisonono) na ulevi wa kupindukia. Mtafiti mmoja aliyeitwa Georges Cuvier ambaye aliwahi kufanya kazi na Sarah hapo Paris, alichukua mwili wa Sarah akaupasua na kutoa vitu vya ndani kama viungo vya uzazi, na jinsi zake na kuziweka katika chombo cha kioo kama jagi na kuvionesha katika jumba la Makumbusho ya vitu vya asili jijini Paris. Pia Georges alihifadhi mifupa na fuvu lake (Skeleton) na ubongo wake pia. Kuanzia kipindi hicho, viungo vya Sarah viliendelea kuwa kama maonesho hadi mnamo mwaka 1974, hakika huu ni unyama wa hali ya juu na kuna muda unawaza hivi anawezaje kumfanyia binadamu mwenzie kitendo kama hicho.
Jarida za sayansi yenye kutoka ushahidi wa kibaguzi zilichapishwa kuelezea asili watu weusi, kuwa watu weusi ni tokeo la binadamu jamiiana na sokwe, majibu haya yalitolewa baada ya kufanyia utafiti mwili wa Sarah. Dah.... Baada ya Uchaguzi Afrika ya Kusini 1994 Nelson Mandela kushinda, aliomba mabaki ya mwili wa Sarah kurudishwa Afrika ya Kusini, katika ardhi yake ya asili ili apewa mazishi ya heshima. Serikali ya Ufaransa ilikubali na kufanya hivyo mnamo mwaka 2002 Agosti.
Mabaki ya mwili wa Sarah yalizikwa eneo la Hankey, baada ya miaka 192 tangu Sarah apelekwe Ulaya. Tangu kifo chake kumekuwa na vitabu vingi sana vikiandikwa kueleza maisha yake. Amekuwa kama kielelezo cha kueleza uhalisia wa maisha ya wanawake wengine Jamii za watu weusi duniani, mateso yao na manyanyaso yao duniani kote. Huyu ni Sarah, mwanamke aliyeteseka maisha yake yote, kufanywa chombo cha starehe, hata baada ya kifo chake, bado mabaki yake yalidhalilishwa zaidi ya miaka 100. Tujitafakari sana watu weusi, historia haijawahi kuwa upande wetu, tuna kazi ya kufanya..