Makala

OMAYRA SANCHEZ

OMAYRA SANCHEZ

Imewekwa na Hussein Molito - February 1, 2020

OMAYRA SANCHEZ

Kisa chake kilianzia wapi hasa?...

Armero kwa sasa ni manispaa huko Tolima, nchini Colombia. Miaka ya ‘80 Armero ulikuwa ni mji mdogo tu ila uliojengeka vya kutosha. Hospitali, shule, kanisa kubwa, majengo ya makubwa ya ofisi za serikali na binafsi, viwanda vya kati na maduka ya hiki na kile tayari vilikwishaupamba mji wa Armero.

Kando kando ya mji huu kulikuwa vijiji vidogo vidogo vilivyosheheni mashamba ya pamba. Mashamba hayo yaliyoshamiri barabara, yaliunakshi vyema mji wa Armero na vitongoji vyake kiasi cha kupachikwa jina la ‘Jiji jeupe.’

Mlima Andes wenye safu ndefu sana inayokatiza nchi kadhaa ikiwemo Colombia, ni moja ya vivutio vikubwa eneo la Tolima. Kama ilivyo ada, kwenye milima mirefu, huwa kuna vilele huku na kule vyenye volkano.
Mimi hupenda kuviita vilele hivi viota.

Hapa kwetu, mlima Kilimanjaro una Kibo, Mawenzi na Shira. Vivyo hivyo kwenye safu ya milima ya Andes, moja ya kiota chake chenye volkano kinaitwa Nevado del Ruiz. Kiota hiki kinapatikana Tolima, Colombia. Na ndani ya Tolima ndiko iliko Armero. Hiki Kilele a.k.a kiota cha volkano cha Nevado del Ruiz kiko Kilometa 48 (wengine husema ni kilometa 74) kutoka ulipo mji wa Armero.

Wakati huo, watu waliokuwa wakitoka Armero mjini kuelekea ilipo Nevado del Ruiz walikutana na mashamba ya pamba, makazi ya watu; watu wenye furaha zao, wenye shughuli na mihangaiko yao. Walipishana na chemichemi, vijito na mito iliyotiririsha maji na kunawirisha kijani kibichi kilichovutia zaidi.

Kwa mbali, mwinuko wa Nevado del Ruiz ungeonekana ukiwa umetandwa na moshi, theluji pamoja na ule ukijani uliozunguka eneo zima la chini la mwamba. Palivutia mno, palivutia sana.

Ni nini sasa kilitokea?...

Siku chache kabla ya Novemba 13, 1985. Kulitokea mitikisiko ya hapa na pale eneo lenye volkano. Kabla ya hapo, tayari taarifa kutoka mamlaka za hali ya hewa nje na ndani ya Colombia zilitoa tahadhari na kuiomba serikali ya Colombia kuwahamisha watu waliokuwa wanaishi karibu na eneo la Nevado. Tahadhari ile ilipita tu kama sauti, haikutiliwa maanani kwa vitendo.

Mara kadhaa watafiti walifika eneo husika na kuondoka wakiwa na wasiwasi mkubwa kuwa kuna hatari ilikuwa njiani. Waliitaja mpaka miji iliyopaswa kukimbiwa ikiwemo Armero. Lakini, hakuna kilichofanyika. Inasemekana Meya wa Armero alilihangaikia sana jambo hili lakini Gavana wa Tolima alimpuuza tu.

Wananchi waliambiwa watulie tu, kwamba hakukuwa na hatari kubwa yoyote.

Sasa usiku wa saa tatu hivi, Novemba 13, 1985 wakazi waliokuwa karibu na Nevado, walishuhudia miale ya radi, ngurumo za kutisha na mtikisiko mithili ya tetemeko la ardhi kutoka kule kwenye eneo lenye volkano.

Kilometa nyingi kule ulipo mji wa Armero, kadhia hizi zilisikika pia ila si kwa kiwango cha kuwatisha. Wengi walioamka muda huo walirudi kulala na waliokuwa katika shughuli zao, waliendelea na yao.

Ghafla, vishindo mfululizo vilipasua anga. Mvua kubwa sana ilianza kunyesha. Volkano ilikuwa imelipuka kwa kiwango cha kutisha kabisa. Theluji iliyochanganyikana na tope la moto sana pamoja na vipande vya miamba viliruka na kuteremka kwa kasi kutoka Nevado.

Mchanganyiko wa haya yote ulishuka kwa kasi ya ajabu mno. Kasi kali sana labda kwa sababu ya ile mvua kubwa; Ukasomba miti na kila kitu kilichokuwa mbele yake kuelekea kwenye vijito.

Hali ile iligeuka kuwa kama mafuriko ya tope zito liendalo kasi lenye makoroko kibao. Mafuriko hayo yalipoingia kwenye makazi ya watu yalisomba nyumba, mashamba, madaraja, magari, miti, wanyama na watu.

Kwa namna yalivyokuwa yakija kwa kasi, na namna huduma ya mawasiliano ilivyokuwa miaka hiyo, wakazi wengi wa Armero hawakujua kilichokuwa kinaendelea milimani huko.

Wachache mno waliopata taarifa kwa kupigiana simu na kujaribu kukimbia makazi yao waliokoka. Wengine walitoka na magari yao ila kwa kiwewe waligonga watu barabarani katika harakati za kujiokoa.

Katikati ya kiwewe kile cha kujaribu kukimbia, mafuriko ya tope zito la moto yaliwafunika bila huruma.

Ilichukua muda wa saa mbili tu kwa Volkano kulipuka na kuuzamisha mji wa Armero kwa asilimia 85.

Watu zaidi ya 23,000 walikufa katika mlipuko huo na vijiji 13 vilifyekwa kama mzaha.

Ni asimilia tano tu ya wakazi wa hapo ndiyo waliookolewa wakiwa na majeraha ya kutibika na wengine yakiwaachia vilema vya maisha, achilia mbali kuathirika kisaikolojia.

#Omayra_Sanchez…

Akiwa miongoni mwa watu waliokumbwa na mafuriko haya, Omayra alikuwa msichana wa miaka 13 tu wakati huo. Siku ya tukio Omayra alikuwa na kaka yake pamoja na shangazi yake. Mama yao alikuwa amesafiri kwenda mjini Bogota kibiashara.

Kadhia zote za mtetemo, ngurumo na pilika zingine za kuomboleza walizisikia. Hakukuwa na namna ya kutoka na kukimbia. Uwe nje uwe ndani tope lingekufikia tu. Tayari walishazungukwa na mafuriko na sasa walijikunyata ndani wakisubiri tu kusombwa. Nyoyo zao zilijaa hofu ya kifo.

Ghafla nyumba yao ilipigwa kwa kishindo na kila kitu kutawanyika. Hekaheka za kujinasua kutoka kwenye tope wakati nyumba ikititia na kuzama zilipamba moto. Kila mtu alipambana kivyake.

Baada ya muda kupita, tuseme saa kadhaa, Omayra alijikuta akiwa amenasa kwenye tope ambalo chini yake ndiko nyumba yao ilikotitia na kutawanyika. Alifunikwa hadi shingoni na takataka nyingi mbali na tope lenyewe.

Waokoaji waliokuwa wameshaanza kufika eneo la tukio, waliuona mkono wake ukiwa umekamata kipande cha mti mwembamba. Walijaribu kumnasua. Wakamfukua hadi kiunoni, wakaishia hapo. Kwa kuwa haikuwezekana tena kumtoa zaidi.

Kila walipomvuta hakutoka. Mbaya zaidi, maji yaliyojitenga na tope yalianza kuja juu. Walihofia angezama, hivyo wakamvalisha tairi ili asizame zaidi. Haikusaidia, maji yaliendelea kuja juu polepole.

Eneo zima lilijaa vilio vya hofu, maumivu na kuomba msaada. Vifaa vilikuwa duni mno, na waokoaji walikuwa wachache mno kulinganisha na idadi ya watu waliokuwa wakihitaji kuokolewa. Helkopta mbili tatu zilizobeba majeruhi hazikutoshea hata kidogo.

Ajabu, Omayra alikuwa mwenye matumaini sana. Katikati ya hali ile aliimba, alizungumza na waokoaji, alikubali kuhojiwa na mwandishi wa habari. Aliomba kupewa maji, biscuit au soda. Alikuwa mwenye matumaini ya kutoka pale. Kwake yeye kuwa mzima baada ya kusombwa na tope lile kulimaanisha uhai. Alitaniana na kucheka na waokoaji waliokuwa wakitafuta namna ya kumtoa.

Muda zaidi ulikatika bila mafanikio, waokoaji waligundua hawawezi kumtoa Omayra pale alipokwama. Ilionekana miguu yake ilikuwa imejikunja huko chini mithili ya mtu aliyepiga magoti. Njia pekee iliyoonekana kufaa ilikuwa kuikata miguu ya Omayra ibakie huko chini na yeye atolewe.

Tatizo likawa, wangemkata na nini hasa? Wangemkataje katika hali ile na mazingira yale?

Ilikuja kugundulika baadaye huwa marehemu shangazi yake aliyekuwa chini huko akiwa amebanwa na matofali ya nyumba na mbao alikuwa ameikumbatia miguu ya Omayra kwa nguvu mno mno mno. Ndiyo sababu ya Omayra kukwama akiwa amepiga magoti.

Taratibu uchangamfu wa Omayra ulianza kupotea. Hofu ya kifo ilianza kumvaa. Maumivu yalianza kuzama mwilini mwake. Alianza kulia na kusali kwa sauti. Hii iliongeza simanzi zaidi. Waokoaji hawakujua wafanye nini tena kumsaidia. Iliumiza mno kushuhudia kutetereka kwake.

Saa zikazidi kuyoyoma Omayra akiwa vile vile, pale pale. Kila walipojaribu kumvuta maji yalikuja juu naye akadidimia kwenda chini zaidi. Mikono yake ikaanza kufa ganzi na kupata rangi nyeupe. Akaanza kuchanganyikiwa na kupayuka. Kuna nyakati aliomba wamtoe kwa kuwa angechelewa shule na kuadhibiwa.

Hali ilipozidi kuwa tete, Siku ya tatu tangia kunasia pale ardhini, rangi ya mwili mzima iligeuka kuwa nyeupe na macho yake yalianza kuvilia damu, wakati huu Omayra aliacha kulia na kutapatapa, alianza kuaga watu akiwemo mama yake ambaye alikuwa mbali na upeo wa macho yake. (Ipo video aliyorekodiwa akitamka kwa heri mama.)

Ni kama vile maumivu aliyokuwa anayasikia yalikuwa makali mno. Alikuwa ameteseka kwa takribani saa 60! Karibia siku 3 za mateso makali!!

#Frank_Fournier...

Mwandishi huyu wa habari na mpiga picha wa Kifaransa alifika Armero alfajiri baada ya safari ya gari ya muda wa saa tano na kuchapa mwendo wa miguu kwa saa mbili na nusu akitokea Bogota. Alipolifikia eneo la tukio aliishiwa nguvu. Hali ilikuwa mbaya kuliko alivyokuwa akifikiria akiwa njiani kuelekea huko.

Alivisikia vilio vya watu waliopigania pumzi za mwisho. Ilitisha, ilisisimua katika namna ya kuogofya. Akiwa amepigwa na butwaa, mkulima mmoja alimuita na kumwonyesha mahali alipo Omayra Sanchez.

Alimkuta peke yake wakati huo, waokoaji walikuwa wanahangaika kusaidia watu wengine pia. Wafanyakazi wachache wa Red Cross walikuwa wamejaribu kuomba kuletewa pump ili kufyonza maji yaliyokuwa yanapanda juu pale alipokwamia Omayra. Ombi lao halikutekelezwa.

Frank anasema, alijihisi asiye na msaada wowote alipomtazama Omayra. Alivutiwa na namna alivyokuwa katika hali ya kujiamini na kuamini angetoka pale salama. Akiwa hapo alishuhudia pia hali ya Omayra ikibadilika na kuwa mbaya. Aliyashuhudia machozi ya maumivu, na namna mwili wake na macho yake vilipoanza kuvilia damu.

Pamoja na yote, dakika za mwisho ngumu na chungu mno kwa Omayra zilikuwa zenye utulivu wa ajabu.

Msaada pekee aliouwaza ni kujaribu kutunza kumbukumbu za nyakati za mwisho za binti huyu. Alimpiga picha huku roho ikimuuma mno. Alifikiria tu pengine picha hiyo ingetoa mwamko kwa serikali na watu nje ya Armero kuwahisha misaada.

Omayra aliwakilisha maelfu ya watu wazima na watoto waliokuwa wamekwama kwenye tope zito na kufariki pasi msaada wowote. Ndivyo ilivyo hata sasa Omayra amebaki kuwa kielelezo cha janga hili!

November 16, 1985 saa 3:45 asubuhi Omayra alifariki dunia. Ikiwa ni saa tatu tu tangu Frank awasili eneo la tukio na dakika chache tu baada ya kupigwa picha.

Picha ilipokwenda hewani ilipokelewa kwa mitazamo tofauti juu ya maadili ya upigaji picha za habari. Wapo waliomsifu Frank na wapo waliomkosoa vikali sana.

‘Ni kwanini hakumsaidia kwanza kabla ya kumpiga picha?’ lilikuwa swali kuu. Waliokuwa mbali na eneo la tukio hawakuelewa hali halisi ilivyokuwa.

Picha ya Omayra iliyopigwa na Frank pamoja na kuamsha mijadala mikubwa kuhusu tukio hilo na uzembe uliofanyika katika uokozi, pia, mwaka 1986 ilishinda tuzo ya picha ya mwaka.

Frank anasema, kuna wakati matukio hayapewi uzito yanapozungumzwa bila picha kuonyesha uhalisia. Bila ile picha dunia ingeendelea kukaa kimya, pengine isingeyahisi maumivu yoyote ya watu waliokufa Armero. Yeye binafsi, kushuhudia tukio lile kulimtesa mno maishani mwake.

Mama yake Omayra alibaki na kaka wa Omayra ambaye yeye aliokolewa akiwa amekatika kidole. Pengine kama si shangazi kuibana miguu ya Omayra kule chini, binti pia angeokolewa.

Armero ya sasa…

Ikiwa inaelekea kutimia miaka 35 tangu kutokea kwa tukio hili la kutisha. Mji wa Armero umebaki kama mji mfu iliotengwa kwa ajili ya ‘Dark Tourism’ Yamebaki magofu yaliyotitia, vichaka, miti mirefu, makaburi kila kona na ukimya unaosisimua.

Wafiwa hurudi kufanya ibada kwa ajili ya ndugu zao. Watalii hutembelea kujifunza. Ni mji unaoleta majonzi hata kwa kuutazama tu. Kuna eneo la ibada lililotengwa kwa ajili ya kumkumbuka Omayra. Kuna kituo cha makumbusho.

Inasemekana serikali ilishindwa kutoa msaada itakiwavyo kwa sababu jeshi lilikuwa limekusanyika mjini Bogota kwa ajili ya kupambana na kikundi cha waasi nchini Colombia kiitwacho Leftist Guerrillas.

Siku tatu nyuma kabla ya mlipuko wa volkano, kikundi hiki kilivamia mahakama na kuua mahakimu 12 kwa mpigo. Tukio hili liliitetemesha nchi vibaya mno, hivyo nguvu kubwa ilielekezwa kwenye kuwasaka wahalifu kuliko kwenda kuokoa wahanga wa Armero.

Inasemekana pia, Meya wa Armero alikufa akihangaika kumpigia simu Gavana wa Tolima ambaye alikuwa akicheza pool wakati maafa yanatokea. Alikataa katakata kuipokea simu ya Meya, akimuita Meya chizi wa Armero bila kujua safari hii haikuwa simu ya kuomba msaada wa kuhamisha wakazi ila msaada wa kuokolewa.

Kuna vitabu vinaizungumzia Armero, viko katika lugha ya kihispania.

Mpaka leo kuna watu wanawatafuta watoto na ndugu zao. kuna watu hawajui walipo wanafamilia wenzao. Kuna watu wanaishi kwa hofu mno sababu ya kile walichokishuhudia.

Hii ndiyo Armero iliyotitia na maelfu ya watu na kuacha kumbukumbu za kuhuzunisha kama za Omayra Sanchez.

Hata leo hii majengo yaliyosalia yametitia kama yalizozama kidogo. kuna habari za mizimu kuonekana na sauti za watu wasioonekana kulia kwa uchungu.

Laura Pettie
30 Jan, 2020
Kigamboni