Makala

KAMWE USIBADILI MTAZAMO WAKO

KAMWE USIBADILI MTAZAMO WAKO

Imewekwa na Mr Hadithi - April 28, 2019

   Katika maisha ya wanaadamu, tumejaaliwa akili thabiti na muumba wetu ambayo kila kukicha tunapigania katika kuijenga dunia iliyo bora. Dunia ambayo ni rafiki kwa maisha ya mwanadamu katika nyanja zote.

   Ndo maana kwa sasa hatutumii miaka mingi kusafiri kutoka sehemu mojja kwenda sehemu nyngine kama zamani baada ya wanaadamu kuzitumia akili vyao vyema na kuunda magari, ndege, treni, meli na kadha wa kadha katika kuhakikisha dunia inapendeza na kuwa sehemu nzuri ya kuivunia kuishi.
  
   Siku hizi tunasafiri kutoka hapa nyumbani mpaka China kwa masaa kumi na nane tu, ilihali kwenye vitabu vya dini tuliwasoma Mitume iliyopita wakitumia miaka mingi njiani wakiwa na usafiri wa ngamia na farasi pekee.
   
   Kila leo umri wa kuishi duniani (life span) ya mwanadamu  inashuka. Hadi sasa inakadiriwa kua umri wa mwanadamu kuishi kwenye uso wa dunia ni miaka 65 mpaka 80.

   Hivyo jaribu kuchkua miaka 65 kisha  toa kwa miaka ulionayo, angalia umebakisha miaka mingapi kwa makadirio. Kisha jiulize, umefanya nini kwenye dunia hii ambacho kama si dunia basi hata familia yako itakukumbuka na kujivunia uwepo wako kwenye uso wa dunia?

   Maana kanuni ya maisha ni  tunazaliwa, tunajenga, tunakufa. Sasa jiulize  ni kipi ulichojenga kwenye dunia kwa manufaa ya kizazi kijacho kabla uhai wako hujafikia kikomo?

   Muumba wetu amemjaalia kila kiumbe wake bila kuchagua dini wala kipato, upeo wa kufanya mambo makubwa kwene sayari hii tofauti na mwengine yeyote yule. Ndo maana mimi na wewe hatufanani uwezo hata kama tunasomea kitu kimoja. 

   Mimii naweza kuitumia kalamu yangu vizuri kwenye kuandika. Kuna mwengine anaweza kuitumia sauti yake  vizuri kusoma nilichokiandika. Na wote kwa pamoja tukaingiza kipato kupitia sanaa zetu.

   Lengo ni kusimamia  MSIMAMO wa kila kitu ulichojiwekea kufanya kwenye maisha yako. Iwapo unahisi ni kitu fulani una uwezo wa kufanya, basi simamia hicho kitu kwa kila hali. Kutokua bora kwenye kitu hicho haimaanishi ukiache, bali wekeza kwenye elimu kwakufuatilia watu waliofanikiwa kwa kufanya vitu hivyo. Amini unayo nafasi ya kuongeza kitu kipya ambacho mwanadamu mwengine hajawaza kufanya hivyo. Unaweza kuwa sehemu ya kumbukumbu nzuri kizazi na kizazi kwa vitu ulivyovifanya kwa moyo.

   Wengi hua tunafeli kwa kua hua hatuhitaji kufanya mambo makubwa. Hua tunaridhika pindi tupatapo hela ya kula na hatuthamini vipawa tulivyopewa na Mungu  katika kuendelea kuijenga dunia yake.

   Dunia bado haijatosheka  na vitu vilivyomo. Hivyo bado unayo nafasi ya  kufanya kitu kipya au kuendeleza yale waliyofanya watu waliopita.

   Ndio maana mpaka sasa bado tunanukuu maneno ya wanafalsafa wa zamani kwa kuhisi walitabiri mambo yatakayotokea mbeleni. Kumbe hata kwa haya maandishi naweza kuja leta ufumbuzi wa matatizo mengi huko mbeleni na yakaishi miaka elfu mbili huku mimi mwenyewe nikiwa nimeishi kwene uso wa dunia chini ya  miaka mia.

   Kutokua na msimamo kumetupelekea vitu vingi kuvifanya nusu kama si kubaki na wazo tu kichwani bila kulitumia. Halafu akitokea mtu mwengine akilitumia na kufanikiwa ndipo hukumbuka kua hata wewe ulikua na wazo kama lile.

   Nakumbuka miaka ya nyuma kuna msanii wa kizazi kipya (jina kapuni) alikua na msemo aliopenda kuutumia kwenye nyimbo zake. 
"wasanii sasa tunatosha wengine wabaki ushabiki."
Alisahau kua masikio hayatosheki kusikia na macho hayashibi kuona. Hivyo kila  mtu anayo nafasi ya kuimba na kusikilizika iwapo tu atakuja na kitu chenye kushawishi watu kumshabikia.

   Hivi tunavyoongea msanii huyo bado anaishi, ila wale  ambao aliwakatisha tamaa enzi hizo wanaishi maisha mazuri mara elfu yake kupitia sanaa hiyo.

   Katika maisha jaribu kujifunza kuheshimu thamani ya mtu mwengine. Ili na wewe thamani yako ijulikane. Ukishajua umekuja duniani kwalengo gani, basi utaheshimu kila mtu na kujali muda. Maana malengo ya mja hutimia  pale tu atakapojitambua. 

   Kamwe usibadili msimamo wako eti kwakua mtu fulani amefanikiwa kwa kupitia kitu ambacho hapo awali  hukuwa na mawazo nacho. Maisha ni karatasi ya mtihani na kila mja  ana maswali yake tofauti. Fanya yako kwa bidii ili utusue na dunia ikikukumbuke hata kipindi ambacho hautakuwepo.

NIWATAKIE SIKU NJEMA.