MOLITO

MOLITO

Imeandaliwa na:  Hussein Molito
Gharama (TSHS.) : FREE
Kundi : Maisha
Ukubwa : 224.00 kB

Katika kipindi cha makuzi yangu, nilibahatika kukutana na wasichana wengi warembo. Wapo walionivutia na kufanikiwa kuwa nao karibu.japo kiurafiki wa kawaida. Na wapo ambao hata salamu yao tu sikufanikiwa kuipata. Wapo ambao niliishia kuwasifia kwenye mitandao ya kijamii. Wapo ambao nilifanikiwa kukutana nao baada ya kujuana kupitia mitandao hiyo. Wapo ambao nilifanikiwa kuanzisha nao mahusiano ya kimapenzi na mpaka tunaachana hatukuwahi kuonana. Kiufupi nawapenda sana wasichana wazuri. Sio lazima niwe nao kimapenzi, hata nikiwa karibu nao tu hua nafurahi. Mimi pia ni mfuasi mzuri wa picha. Napenda sana kuweka kumbukumbu. Toka nilipokua mdogo, nilikua naweka miambilli miatatu kisha akipita mpiga picha basi nalipia huduma hiyo kwa pesa yangu. Katika albamu yangu ya picha. Kulikua na picha nyingi sana za watu mbalimbali hususani watoto wenzangu. Ila kilichokuja kunishtua baada ya kutilia maanani utazamaji wa picha hizo za utotoni, nilibaini kitu ambacho kinsnifanya nifurahi kila nipitashapo macho yangu kwenye albamu hiyo. Ni vile nilivyokua napenda kukaa karibu na watoto wa kike toka kipindi ambacho sina ufahamu sawasawa. Yaani mapozi yangu yote lazima nitamshika mtoto wa kike mkono,bega au kiuno. Hata nisipomshika basi nitakua nimegusana nae kivyovyote vile. Hua nacheka nikikumbuka matukio hayo ya utotoni. Maana yananipa tafsiri kua nimekua mkubwa na tabia yangu niliyokua nayo toka utotoni. Tabia ya kupenda wasichana. Sema kwa sasa kidogo nimeongeza kipengele. NAPENDA WASICHANA WAZURI. Mnamo mwaka 2010 ndio mwaka nilioanza kujitegemea huku nikisubiri matokeo yangu ya kidato cha nne. Miezi mitatu kilikua ni kipindi kirefu sana cha kusubiri mpaka matokeo yatoke. Hivyo kwa sisi tuliotoka shuleni ni kazi sana kukaa nyumbani bure bila kuingiza kitu chochote. Maana hata kile kiasi cha pesa kidogo tulichokua tunapewa na wazazi wetu wakati tunaenda shuleni kilikua kimekomea hapo. Ili kupambana na ukame wa pesa, ilinibidi nitafute kazi kama si kibarua cha kunishikiza wakati nasubiri matokeo yangu ya kidato cha nne. Sikua na hofu kubwa ya kufeli kutokana na jinsi nilivojaza majibu yangu kwa kadri niwezavyo. Pia sikua na ubavu wa kusema kua nitafaula kwa daraja la kwanza. Niliamini kua nitafaulu daraja la pili kwa asilimia kubwa sana. na hata ikitokea nimeanguka sana basi itakua daraja la tatu. Nalo pia si daraja ambalo nilikua nafikiria kupata kwa vile mtihani ulivokuja kwenye njia zangu nilizosoma wakati wa mwishoni.. Kizungu tunaita 'Final Touch'. Ila kwa upande mwengine wa shilingi kwakua mtihani ni mtihani...niliweka imani tu moyoni ili kukabiliana na matokeo yoyote yatakayotoka. Katika mahangaiko yangu yangu ya kutafuta kibarua, nikafanikiwa kuonana na kijana mwenzangu. Japo yeye alinitangulia umri kwa miaka kadhaa. Ila kwa jinsi alivojiweka, sikuweza kumpa shikamoo zaidi ya salamu zetu za vijana. Nakumbuka jina lake anaitwa Sebastian. Jina la utani alikua anajiita Mwarabu wa Misri. Hivyo alijibatiza jina na kujiita Al-Hadaad. Huyo kijana alinipatia ajira ya kumuandika bango lake baada ya kufungua ofisi ya kukodisha mikanda ya filamu. Kwakua nina fani nyingi na uchoraji ni moja ya fani iliyonipa umaarufu sana mtaani kwetu, nilimtajia bei zangu mbalimbai hasa kulingana na huduma anayotaka na baada ya maafikiano nikaenda kununua rangi na brashi kisha nikaifanya kazi yake. Alivutiwa na kazi niliyoifanya na kunipa ujira wangukama tulivyokubaliana hapo awali. hivi unamjua kijana yeyote mjanja mjanja ambaye anaweza kutumia computer vizuri, Akawarushia watu nyimbo kwenye simu na kuchoma CD?..... Nataka nimuache hapa ofisini maana mie nipo bize na mambo mengine Kauli hiyo kwangu ilikua ni kama nyota ya Jaa. Maana sikuremba mwandiko, niliweza kumuambia kua hata mie naweza hiyo kazi na kipindi hicho nilikua tu nyumbani baada ya kumaliza masomo yangu ya kidato cha nne. Basi bila hiyana bosi wangu huyo akanipatia ajira nyingine. Ajira ngeni ambayo sijawahi kuifanya hata siku moja kwenye maisha yangu. Hiyo computer yenyewe nilikua naishia kuiona tu ila kiukweli sikuwahi kutumia. Hata kibonyezeo cha kuwashia tu nilikua sijui kinakaa wapi. Hivyo niliongopa kua mie ni mtaalamu wa kifaa hicho ilimradi tu nipate kazi. Eeh, maana hata kinyozi hujifunzia kwenye vichwa vya watu. Cha msingi ni usiri wake na kujiamini tu ndio kunamfanya afanye kazi nzuri na mteja kumlipa na kumsifia kwa kumpendezesha bila kujua kua hata huyo inyozi moyo ulikua unamdunda wakati anaifanya kazi hiyo. Kwakua hata Al Hadaad mwenyewe alikua hajui lolote kuhusiana na Computer, niliwasiliana na kaka yangu wa mtaani. Anaitwa Julius Semindu. Huyu ni mmoja kati ya watu walionipa somo la kuijua Computer kwa siku moja tu. Kwanza aliniambia computer ina mambo mengi sana. Yahitaji miaka dahri kujifunza na sidhani kama utaweza kujua kila kitu. Maana kila siku yanaongezeka mambo mapya. Ila ni rahisi sana kuitumia pindi pindi utakapojua wewe kama wewe unahitaji kujua kitu gani. Maneno yake yalinikaa kichwani na nikaweza kugundua kua mimi sihitaji kujua vitu vingi kwenye mattumizi ya kifaa hicho. Ila nahitaji kujua jinsi ya kuwasha, kuzima, kuchoma CD na kurusha nyimbo kwenye simu. Kwa kutumia computer yake, alinielekeza vitu hivyo. Na alipofika ofisini kwangu na kuiona computer mpya ambayo bosi wangu ameninunulia, ilikua haina programu za kuweza kufanya kazi nilizoorodhesha kuhitaji kufundishwa. Haikua na nyimbo pia. Aliniwekea hizo program na kunieleza jinsi ya kuziweka pia. Pia alichukua kifaa chake alichonijulisha kwa jina la External Disc na kunijazia nyimbo chache zilizokua humo. Kwa mara ya kwanza nikaona kumbe kutumia Computer ni rahisi, nilikua niogopea bure tu hapo awali. Nikaanza kuitumia kwa kasi. Nakumbuka mara kadhaa niliamua kukesha ofisini na sirudi nyumbani kwa kucheza magemu ambayo hapo awali nilikua nalipia kwenye vituo vya playstation. Baada ya mwezi mmoja tu kupita, nikawa fundi. Nilikua naweza mpaka kubadilisha window. Bado nikawa najua matatizo ya Computer na kuna baadhi ya watu waliniita fundi Molito wengine Mr. Computer Solution kwakua niliweza kuwarekebishia Computer zao. Uchangamfu wangu ulinifanya nitengeneze marafiki wengi na kujipatia wateja wengi pia. Niliweza kumshinda hadi mpinzani wangu ambaye ndiye alikua anatamba kwa kukodisha CD eneo hilo. Wateja wengi waliokua wanakuja ofisini kwangu walikua wananisifia na kuniambia kua mimi ni mpole na sina Dharau kama alivyo mpinzano wangu kwakua alitangulia eneo hilo lililokua na uhaba wa maktaba hizo za mikanda. Sikua mvivu wa kufuatilia CD ninapozikodisha na kuna baadhi ya wateja ambao kwao pesa sio tatizo. Kila CD mpya ikitoka nilikua nawapelekea wao kwanza nyumbani. Siku moja nikiwa ofisini. Mishale ya saa tatu baada ya kupata kifungua kinywa nikawa napanga CD zangu. Maana nilikua naipenda kazi yangu vilivyo. Kuna wakati nilikua napata pesa mara nne ya kiwango cha pesa alichoniwekea bosi wangu kwa wiki. Hivyo hata kimuonekano nikaanza kupendeza. Usafi wangu kimavazi ukawa kivutio hadi kwa wasichana. Na wengine hawakusita kunisifia bila kuficha. Molito jamani.... Umetoka waaaoooh Nilitabasamu na kushukuru kila nigunduapo kua nilikua nastahili kusifiwa kwakua nilikua naenda na wakati. Wakati huo tulikua tunaita kuripuka pamba. Nikiwa katika kupangapanga vitu vyangu vizuri na kufuta vumbi, nilisikia sauti nzuri ikinisalimia. Ni sauti niliyohisihi imetokea puani. Niliunyanyua uso wangu na kumtazama msichana huyo aliyesalimia. Hamadi! Nilikutana na sura ngeni ya Malaika imesimama mbele yangu. Msichana mzuri hasa ambaye kwenye kumbukumbu zangu sidhani kama nilishawahi kumuona hapo kabla.